Uongozi wa Wilaya ya Kilosa umeushukuru uongozi wa taasisi ya World vision kwa mchango wao ambao wamekuwa wakiutoa kupitia miradi mbalimbali ambayo wamekuwa wakiifanya katika sekta ya elimu, afya, maji,kilimo, uchumi, uongozi, maendeleo pamoja na ufadhili wa watoto.
Shukrani hizo zimetolewa Oktoba 6 mwaka huu na Katibu Tawala Wilaya Yohana Kasitila wakati akipokea madawati 100 kwa ajili ya shule ya msingi Mtumbatu pamoja na kadi za bima kwa watoto 2,910 pamoja na cherehani 35 kwa ajili ya vijana waliojifunza ujasiriamali vyote vikiwa na thamani ya shilingi 31,475,000.
Kasitila amesema kazi iliyofanywa na World Vision ni kubwa kwa ajili ya maendeleo ya wanakilosa na inastahili kupongezwa kwani vifaa hivyo vitakuwa msaada mkubwa hususani kwa kizazi cha sasa na baadaye na kwamba vifaa hivyo vimepunguza changamoto ya wanafunzi kukaa chini lakini pia upande wa vyerehani vitakwenda kuwasaidia vijana kujitegemea na kujikwamua kiuchumi huku kadi za bima zitasaidia watoto kupata huduma za afya bila usumbufu.
Aidha ametoa rai kwa Serikali ya kijiji na wananchi kiujumla kuwatazama wazee na wasiojiweza ili waweze kupata bima ya afya na kwamba ili uchumi kuimarika unahitaji watu wenye afya bora na elimu hivyo ipo haja ya wananchi kujipanga namna ya kuendeleza mema yote yaliyofanywa na World Vision ambao wanatarajia kumaliza muda wao ifikapo tarehe 30/09/2021.
Naye mwakilishi kutoka World Vision Bw. Kulanga amesema kutokana na kutambua juhudi zinazofanya na Serikali World Vision imejikita katika kuunga mkono juhudi hizo hususani kwa kuboresha miundombinu ya shule ikiwemo ujenzi wa madarasa, nyumba za walimu na ofisi pamoja na ujenzi wa vyoo, kuijengea jamii uwezo juu ya afya ya mama na mtoto, lishe, usafi binafsi na wa mazingira, uchimbaji na ukarabati wa visima vifupi vya maji, kuwajengea uwezo jamii juu ya mbinu bora za kilimo na ufugaji ili kuongeza uzalishaji na kipato pamoja na kuwezesha upatikanaji wa mbegu bora , pembejeo lakini pia mafunzo ya ujasiriamali, uanzishwaji na uendeshwaji wa vikundi vya kuweka na kukopa na mambo mengine mengi.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa