Zaidi ya watoto 108,000 walio na umri wa kwenda shule wilayani Kilosa Mkoani Mororogo wamepewa dawa kama tibakinga kwa magonjwa ya kichocho na minyoo ambayo yalikuwa hayapewi kipaumbele ili kuwakinga wasiathiriwe na magonjwa hayo.
Hayo yameelezwa Februari 25 mwaka huu na Mratibu wa mpango wa kudhibiti magonjwa ambayo yalikuwa hayapewi kipaumbele Halmashauri ya Wilaya Kilosa Rosemary Nguruwe katika ziara yake ya kutembelea shule mbalimbali za msingi ambazo zilitumika kama kituo cha kumezea dawa na kuona zoezi la umezaji dawa linavyofanyika .
Nguruwe amesema kuwa zoezi hilo limefanyika kwa muda wa siku tatu kuanzia Februari 24 hadi 26 mwaka huu na limekwenda vizuri kwani walimu na wazazi wameonyesha ushirikiano wa kutosha kwa kufanya maandalizi ya kutosha na kuwapa chakula watoto kabla ya kumeza dawa jambo ambalo limepelekea zoezi hilo kuwa na mvuto wa kipekee na kufanya zoezi la umezaji dawa kukamilika katika kila kituo.
Hata hivyo amewapongeza na kuwashukuru walimu kwa ushirikiano wao ambapo amesema kuwa Idara ya Afya na Elimu zinafanya kazi pamoja katika kuihudumia jamii na kwamba kazi kubwa waliyoifanya kuhakikisha watoto wote walioko mashuleni wanameza dawa sahihi kulingana na kipimo, na kuongeza kuwa kwa kazi kubwa waliyoifanya wameisaidia Serikali kupitia Wizara ya Afya kufanikisha zoezi hilo kwani Serikali ina mpango wa kutokomeza magonjwa yote ambayo yalikuwa hayapewi kipaumbele kama vile minyoo na kichocho.
Aidha walimu katika shule mbalimbali akiwemo Mkuu wa shule ya msingi Mkondoa Annastasia Hemed amesema zoezi hilo ni zuri na ni muhimu kufanyika mara kwa mara ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea kupitia magonjwa hayo kwa kuwa linasaidia kuwaondolea changamoto watoto na ndio waathirika wakubwa kutokana na mazingira na vyakula wanavyokula hasa wawapo shuleni hivyo ni rahisi kupata vimelea vya magonjwa hayo, hivyo wameishauri Serikali kutoa dawa hizo mara kwa mara ambapo itasaidia watoto wote kumeza kwa muda muafaka.
Nao wanafunzi kwa nyakati tofauti wameeleza kuwa wanaishukuru Idara ya Afya kupitia Halmashauri ya Wilaya Kilosa kwa kuwathamini na kuwapelekea dawa hizo mashuleni na kwamba hawana uwezo wa kuzipata dawa hizo kwa wakati ukizingatia kwao ni rahisi kupata vimelea vya magonjwa hayo kulingana na changamoto ya mazingira.
Kwa upande wa Madaktari katika vituo vya Afya na Zahanati wamesema dawa hizo hazina madhara yeyote kwa mtoto na kwamba wazazi hawana budi kumpeleka mtoto mwenye sifa katika kituo cha kumezea dawa ili aweze kupata tiba kinga ili kujihakikishia usalama wa afya ya mtoto dhidi ya magojwa hayo.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa