Mbunge wa jimbo la Kilosa kwa kushirikiana na waheshimiwa madiwani wa tarafa ya Magole wametoa shukrani za dhati kwa Serikali ya awamu ya sita kwa namna ambavyo imekuwa ikiitazama Wilaya ya Kilosa kwa jicho la tatu kwa kuhakikisha inawaletea wananchi maendeleo sambamba na kuhakikisha inatekeleza yale iliyo yaahidi wakati wa kampeni za uchaguzi ikiwemo utatuzi wa kero mbalimbali.
Shukrani hizo zimetolewa mwishoni mwa wiki hii wakati wa ziara ya kamati ya CCM Mkoa ilipotembelea tarafa hiyo ili kuzungumza na wananchi ambapo Mbunge wa jimbo la Kilosa Mh Prof. Palamagamba Kabudi amesema Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa ajili ya utatuzi wa changamoto mbalimbali ikiwemo changamoto ya maji ambapo takribani shilingi milioni 97 zimetolewa na Serikali ili kuunganisha kisima cha Matongolo kwenda kwenye tanki la maji.
Aidha Prof Kabudi amewataka wananchi wote kwa aujumla kuendelea kutunza vyanzo vya maji kwa kuhakikisha miti haikatwi hovyo na kuchoma mkaa, kutokakata magugu na mikuyu, jambo linalosababisha kuwa na uhaba wa maji na kwamba kila mmoja ahakikishe miti inapandwa ya kutosha ili kuwepo na upatikanaji wa maji kwani Serikali inafanya juhudi za kuleta maji kwa wananchi ili kuondoa adha ya uhaba wa maji.
Pamoja na hayo ametoa rai kwa wananchi kuzichukua changamoto na kuzigeuza kuwa fursa ya kujiletea maendeleo kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika utatuzi wa changamoto na kwamba changamoto la umeme Serikali imeshatoa fedha kwa vijiji vyote kupewa umeme na kwamba inatarajiwa ifikapo mwezi Disemba 30, 2023 vijiji vyote nchini viwe na umeme na kwamba Serikali imejipanga baada ya kumaliza suala la umeme vijijini itaanza mchakato wa upatikanaji wa nishati safi ya kupikia.
Kwa upande wa madiwani wa kata za tarafa ya Magole ikiwemo Mvumi, Msowero, Kitete, Dumila, Magole, Mbigiri, Mamboya, Maguha, Mabula, Mtumbatu, Magubike na Berega wamemshuru Mheshiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa fedha mbalimbali zilizopelekwa na zinazoendelea kupelekwa kwenye kata zao ili kuwasaidia wananchi ambapo kumekuwa na miradi mbalimbali inayoendelea ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya na zahananti, ujenzi wa shule na miundombinu mbalimbali sambamba na miradi mingine mingi.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa