Wawezeshaji wa mpango wa kunusuru kaya maskini(TASAF) ngazi ya Wilaya kwa kushirikiana na madiwani pamoja na viongozi katika ngazi ya vijiji wametakiwa kuhakikisha wanawatambua walengwa sahihi wa mpango wa kunusuru kaya maskini(TASAF) waliokusudiwa na kuhakikisha kazi hiyo inafanyika kwa uadilifu na uwazi badala ya kuweka wanufaika hewa kwa kuweka majina ama kaya zisizostahili kwani lengo la mpango huo ni kumsaidia mwananchi maskini.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa alhaji Majid Mwanga ambapo amewataka kuhakikisha wanatimiza mwongozo unavyoelekeza na kwamba kila mmoja atambue kuwa anakwenda kuwakilisha Serikali hivyo miradi itakayoibuliwa iwe na mwendelezo ambayo itawanufaisha walengwa na jamii kiujumla ambapo pia ametaka katika shughuli mbalimbali kushirikishwa kwa maafisa tarafa kwani kwa kufanya hivyo itasaidia shughuli hizo kusonga mbele.
Janeth Maduhu ambaye ni mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji TASAF amesema tathmini ya utekelezaji wa mpango wa kunusuru kaya maskini katika kipindi cha kwanza cha awamu ya tatu umepungua kutokana na walengwa kujiimarisha katika kufanya shughuli mbalimbali za kijiongezea kipato na kujiimarisha kiuchumi kwa kufanya shughuli za kilimo, ufugaji, uvuvi na ujasiriamali ambapo awali baadhi ya vijiji vilifikiwa na kwamba katika awamu hii ya pili vijiji vyote vitafikiwa.
Kwa upande wake Waziri wa Katiba na Sheria ambaye pia ni mbunge wa Kilosa Kati Mh. Prof.Palamagamba Kabudi amesema fedha zinazotolewa na mpango huo sio za bure bali kwa ajili ya kuwasaidia walengwa ili kuziondoa kaya lengwa katika umaskini hatimaye waweze kujikwamua na kuchangia pato la Serikali kwani mpango huo umekusudia kuifanya jamii kujikwamua hivyo ni vema washiriki wote watakaoshiriki kuwabaini walengwa kujikita katika uadilifu na uwazi ambapo pia ametaka wananchi washirikishwe katika mchakato huo huku akisisitiza walengwa wote watakaobainika na kuingia katika mpango huo wanapaswa kuzifanyia kazi fedha watakazopatiwa kwa kuhakikisha wanajikwamua na kutoka katika lindi la umaskini kwani mpango huo sio wa kudumu.
Naye mbunge wa jimbo la Mikumi Mh. Dennis Londo amesema ipo haja ya kuongeza umakini na kuzingatia vigezo katika kuwabaini walengwa ili kuboresha utekelezaji wa mpango huo kwa kuwazingatia wanufaika wa masharti ambao watakuwa wamekidhi vigezo ambapo pia amewataka viongozi hao kuhamasisha jamii ili kunufaika na mpango huo kwa kuhakikisha wanatimiza vigezo vyote ikiwemo kupeleka watoto kliniki na watoto wote wanaostahili kwenda shuleni huku akiitaka jamii kutambua kuwa mradi huo sio wa kudumu hivyo ni vema jamii ikapata ushauri mzuri na kuuzingatia ili kuleta mabadiliko kwa walengwanna kuondokana na umaskini.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa