Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi ametoa rai kwa watendaji wote wa kata wilayani Kilosa kuweka maslahi ya Taifa mbele badala ya matakwa yao binafsi katika zoezi zima la utambuzi wa wafanyabiashara walio katika sekta isiyo rasmi kwa ajili ya ugawaji wa vitambulisho vilivyotolewa kwa wafanyabiashara wadogo wadogo ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Mheshimia Rais ambapo uzinduzi wa ugawaji wa vitambulisho hivyo utafanyika tarehe 4 Januari 2019.
Mgoyi amesema kuwa watendaji wote wanawajibika kufanya zoezi la utambuzi wa wafanyabiashara wadogo wadogo kwa kuzingatia uadilifu wa hali ya juu ili kutoingia katika dosari ya aina yoyote na kwamba mtendaji yoyote asithubutu kutumia udanganyifu katika zoezi hilo kwani kwani zoezi linalohitaji uangalifu wa hali ya juu ili kuepuka ukwepaji kodi kwa kuwasilisha majina yasiyostahili huku akiwataka kuepuka rushwa kwani zoezi hili si la kisiasa bali kiutendaji na ni agizo kutoka kwa Rais hivyo libebwe kwa uzito wake na heshima ya Rais na kwamba mtendaji yoyote atakayebainika kufanya udanganyifu sheria itachukua mkondo wake.
Aidha Mgoyi amesema kuwa Wilaya inaendeshwa kwa kilimo hivyo amewataka watendaji hao kuhakikisha maafisa kilimo waliopo katika kata zao wanawajibika ipasavyo ili kwenda sambamba na agizo la Waziri Mkuu la kuwataka Wakurugenzi wote nchini wahakikishe maafisa ugani wawe katika maeneo ya wakulima ili kuwasaidia, hivyo watendaji wanaowajibu kusimamia vizuri maafisa hao na kwamba kila mtendaji anapaswa kuwa na daftari la wakulima ili kuwa na takwimu sahihi za wakulima, mazao yanayolimwa pamoja na hekari zinazolimwa katika maeneo yao.
Akisoma mwongozo wa kugawa vitambulisho kwa sekta isiyo rasmi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmshauri ya Wilaya ya Kilosa Asajile Lucas Mambambale amesema mfanyabiashara anayestahili kupewa kitambulisho sharti awe na mauzo ghafi yasiyozidi shilingi milioni nne (4,000,000/=) kwa mwaka, awe hajawahi kusajiliwa na TRA na kupewa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) isipokuwa wale waliosajiliwa awali na kupata kitambulisho au kama Mlipakodi, anatakiwa ajaze fomu maalum kama mfanyabiashara wa sekta isiyo rasmi mathalan mama lishe, mmachinga na pia mjasiriamali atalipa shilingi elfu ishirini(20,000/=) kwa ajili ya kitambulisho
Sambamba na hayo Asajile amewataka watendaji wa kata kutofumbia macho sekta ya kilimo kani wao ndio wasimamizi wakuu katika maeneo yao katika sekta ya elimu ambapo kwa miaka kadhaa kilosa imekuwa ikishika nafasi ya mwisho kimkoa na kwamba 2019 hatarajii sekta ya elimu katika mitihani ya Taifa kushika nafasi ya mwisho kimkoa na amewataka watendaji hao kukaa na serikali za maeneo yao kupanga mikakati ya kuitoa Kilosa katika nafasi ya mwisho kwa kupandisha kiwango cha ufaulu ili kushika nafasi nzuri kimkoa kwani ni jambo linalowezekana.
Naye Kaimu Meneja TRA Kilosa Musa Haruni ni vema watendaji wa kata na jamii kiujumla ikaelewa kwa kina kuwa walengwa wa vitambulisho hivyo ni wale ambao wanapata mauzo kwa mwaka bila kujali faida wala mtaji wastani wa mauzo ni 11,111.01/= ambapo mauzo kiwango cha chini ni 5000/= huku kikubwa kikiwa 18000/= kwa siku aidha amesema kwa upande wa wafanyabiashara ambao hawajasaliwa na TRA wala hawana TIN lakini ni wafanyabiashara wanaozidi milioni nne kwa mwaka hawapaswi kupewa vitambulisho.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa